Maelfu ya raia wa Iran walikusanyika Tehran tarehe 4 Machi 2026 kuanza hafla ya kumuaga ya siku tatu kwa Kiongozi Mkuu wa Kidini Ayatollah Ali Khamenei, ambaye aliuawa katika mashambulio ya angani na Amerika na Israeli. Mwanawe, Ayatollah Mojtaba Khamenei, anaonekana kama mrithi mzuri huku mvutano wa kikanda unaendelea.
Tarehe 4 Machi 2026, Iran ilianza hafla ya siku tatu ya kumuaga Kiongozi Mkuu wa Kidini Ayatollah Ali Khamenei, ambaye aliuawa Jumamosi akiwa na umri wa miaka 86 katika mashambulizi ya angani yaliyofanywa na Amerika na Israeli. Khamenei alikuwa madarakani tangu 1989, akimrithi Ayatollah Ruhollah Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnamo 1979. Pia alihudumu kama rais wa Iran kutoka 1981 hadi 1989.
Maelfu ya raia walikusanyika Tehran kumpa heshima za mwisho, huku mwili wake ukiwekwa katika ukumbi wa maombi ya Imam Khomeini. Hojjatoleslam Mahmoudi, Mkuu wa Baraza la Kiislamu la Iran, alisema mazishi yatadumu siku tatu na umma utaruhusiwa kuutazama mwili. “Ukumbi huo utakuwa ukiwapokea wageni na raia wa Iran ambao watakuja kumuaga kiongozi wetu wa kidini na kuonyesha Amerika kuwa Iran bado ni taifa imara na halitawainamia,” akasema Mahmoudi.
Mojtaba Khamenei, mwana wa Khamenei, anaonekana kama mrithi anayefaa, lakini viongozi wa kidini hawajatangaza mrithi rasmi kutokana na hofu ya kushambuliwa na Amerika na Israeli. Hii inafanyika huku Iran ikiendelea na mashambulizi ya kisasi, ikiwa ni pamoja na kurusha droni kwenye kambi za Amerika katika ukanda wa Ghuba na kushambulia ubalozi za Amerika huko Dubai na Riyadh. Mnamo Jumanne usiku, droni ya Iran ilipiga eneo la maegesho la ubalozi wa Amerika Dubai, na kusababisha moto na moshi.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Marco Rubio alisema wafanyakazi wote walikuwa salama. Amerika imefunga ubalozi wake Saudi Arabia, Kuwait na Lebanon, na kuwashauri raia wake waondoke nchi 14 za Ukanda wa Mashariki ya Kati. Kamanda wa IRGC Ebrahim Jabari alitangaza kufungwa kwa Mkondo wa Hormuz, akisema, “Mkondo wa Hormuz umefungwa. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kupitia hapo, mashujaa wa Walinzi wa Mapinduzi na jeshi la majini watateketeza meli hizo.” Rais Donald Trump ameapa kulipiza kisasi kwa mashambulizi hayo na mauaji ya wanajeshi 6 wa Amerika.
Mashambulizi ya Iran yamevuruga uchukuzi wa ndege, na mashirika kama Qatar Airways, Emirates na Etihad kuyasimisha shughuli zao.