Iran imesema wataamua wakati vita kati yao na Marekani na Israel vitaisha, huku wakisisitiza hakuna mafuta yatakayosafirishwa nje ya Mashariki ya Kati iwapo wataendelea kushambuliwa. Rais Donald Trump amesema vita vitaisha ndani ya wiki nne au mapema zaidi. Hata hivyo, jeshi la Iran linasema lazima kuwe na mshindi na kauli ya Trump ni upuzi.
Vita kati ya Iran, Marekani na Israel vimeendelea kutoa kauli mbalimbali kutoka pande zote. Iran imesema wao ndio wataamua ni lini vita vitaisha, huku wakihofia usafirishaji wa mafuta katika Ukanda wa Mashariki ya Kati. Taarifa ya jeshi la Iran ilisema, “Sisi ndio tutaamua ni lini vita vitaisha tena kwa njia gani kwa sababu lazima kuwe na mshindi. Kauli ya Trump ni upuzi tu.”
Rais Trump alikuwa amesema vita vitaisha ndani ya wiki nne au hata mapema zaidi kwa sababu Marekani imedhoofisha jeshi la Iran kabisa. Alionya kwamba iwapo Iran itazuia usafirishaji wa mafuta katika Strait of Hormuz, watapigwa mara 20 zaidi kuliko hapo awali. Trump aliongeza, “Tutawashambulia kiasi kwamba itakuwa vigumu tena kwao kuamka au kufufua taifa lao hata kwa msaada wa washirika wao.”
Strait of Hormuz, ambayo inahusika na sehemu ya mafuta yanayosafirishwa ulimwenguni, sasa imefungwa na hakuna meli za mafuta zinazosafiri, hali inayoweza kusababisha kupanda bei ya mafuta ghafi.
Mnamo Jumapili, Iran ilimteua Mojtaba Khamenei kama kiongozi mpya wa kidini baada ya kiongozi mkuu Ayatollah Khamenei kuuawa katika shambulio. Israel imesema vita vitaisha tu iwapo utawala wa kiimla utaondolewa. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema, “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa raia wa Iran wana sauti katika kumchagua kiongozi wao. Mwishowe ni wao ndio wataamua lakini tukifaulu pamoja na watu wa Iran basi tutamaliza kabisa uhasama na vita ambavyo vimekwepo kwa miaka mingi.”
Maafisa wa Marekani wanasema lengo lao ni kuharibu vituo vya nyuklia vya Iran, lakini Trump anasisitiza mabadiliko ya uongozi. Tangu vita vianze mwisho wa Februari, zaidi ya raia 1332 wa Iran wameuawa na wengi kujeruhiwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alisema hawana nia ya kuzungumza na Marekani tena, akisema, “Bado walituvamia wakati mazungumzo yalikuwa yamefikia hatua muhimu. Kuzungumza na Amerika si ajenda yetu tena, huko tumetoka.”