Kocha wa Harambee Starlets, Beldine Odemba, ametajwa kuwa kocha bora wa mwezi Oktoba na Chama cha Wanahabari wa Michezo Nchini (SJAK) wakishirikiana na Betika. Odemba aliongoza timu yake kufuzu kwa michuano ya WAFCON 2026. Kenya itarejea katika dimba hilo baada ya miaka 10.
Beldine Odemba, kocha wa timu ya taifa ya Kenya ya kandanda ya wanawake Harambee Starlets, ametangazwa kuwa kocha bora wa mwezi Oktoba. Tangazo hilo lilifanyika jana na SJAK wakishirikiana na kampuni ya Betika. Odemba alipigiwa kura na jopo la waandishi wa SJAK na kuwashinda wengine kama Kevin Wambua, kocha wa raga wa Shujaa, Musa Benjamin, kocha wa ndondi wa Kenya, Nicholas Muyoti wa Nairobi United FC, Meshack Senge wa magongo, Simon Odongo, kocha wa raga wa Lionesses, na Camilla Lydya, kocha wa taifa wa triathlon.
Odemba aliongoza Starlets kufuzu kwa michunao ya WAFCON 2026 kwa kuwashinda W Gambians 4-1 kwa jumla ya mabao katika raundi ya pili na ya mwisho. Michuano hiyo itachezwa nchini Morocco, na Kenya itarejea baada ya miaka 10 tangu 2016 nchini Cameroon. Kocha huyo mwenye leseni ya ukufunzi ya A alipokea kikombe na hundi la Sh 100,000.
“Tulisubiri sana muda huu ufike. Ningependa sana kushukuru Betika kwa kuwakumbuka wachezaji wa kike na kazi yangu kama kocha. Wachezaji walionyesha njaa ya kutaka kufuzu WAFCON katika kila mechi,” alisema Odemba. Aliongeza, “Haikuwa rahisi lakini tulijiamini na kuhakikisha kwamba tumerejesha Kenya katika WAFCON.”
Bi. Marya Wachira, Mtendaji Mkuu wa Masoko wa Betika, alisema, “Hongera sana kwa kocha Odemba kwa mafanikio haya. Kujitolea kwako na uongozi wako haujawahamasisha tu bali pia umeleta fahari kwa taifa.” Mwenyekiti wa jopo Abuller Ahmed aliongeza, “Ushindi wa kauli moja wa Kocha Odemba ni ushahidi wa uongozi wake bora na kujitolea kwake bila kuyumbayumba. Yeye ni bingwa wa kweli ambaye ameleta fahari kwa Kenya.”
Ushindi huu unaonyesha maendeleo katika michezo ya wanawake nchini Kenya, hasa katika kandanda.