Mamlaka ya Masoko ya Mitaji nchini imesajili mifuko sita mipya ya uwekezaji kutoka Pergamon Investment Bank ili kuwapa Wakenya chaguzi zaidi za kifedha.
Mifuko hiyo ni Pergamon Money Market Fund (KES), Pergamon Money Market Fund (USD), Pergamon Equity Fund, Pergamon Fixed Income Fund, Pergamon Balanced Fund na Pergamon Special Diversified Income Fund. Bi Wanjiru Gichuru, Afisa Mkuu Mtendaji wa Pergamon Investment Bank, alisema usajili huo unaleta suluhu bunifu za uwekezaji na kuchangia ukuaji wa masoko ya mitaji.
Sekta ya mifuko ya pamoja ya uwekezaji nchini imeendelea kukua. Kufikia Septemba 2025, fedha zilizosimamiwa zilifikia takriban Sh679.6 bilioni. Kenya sasa ina zaidi ya mifuko 55 ya unit trust yenye zaidi ya vitega uchumi 230.
Watu kati ya milioni mbili na tatu wanashiriki katika uwekezaji huo kupitia viwango vya chini na usajili wa mtandaoni. Mifuko hiyo imeundwa kulingana na uwezo wa wawekezaji kuvumilia hatari.