Mwanamuziki wa injili Betty Bayo, jina kamili Beatrice Mbugua, alifariki dunia Novemba 10 kutokana na leukemia baada ya kupambana kwa siri na ugonjwa huo. Alificha maumivu yake nyuma ya tabasamu lake maarufu ili kuepuka kejeli mtandaoni. Rafiki yake wa karibu Shiro wa GP alisimulia hadithi ya wiki zake za mwisho zilizojaa uchungu.
Betty Bayo alijulikana kwa nyimbo zake zenye kuinua mioyo na utu wake wa upendo. Dalili za ugonjwa ulianza katikati ya Oktoba, alipokuwa akionekana mchovu kupita kiasi na kukosa nguvu. Mnamo Oktoba 18, alimwambia rafiki yake Mary Wanjiru, maarufu kama Shiro wa GP, kuwa alikuwa akihisi vibaya. Walienda Hospitali ya RFH, ambapo madaktari waligundua kiwango cha chini cha damu na kuvuja damu kupita kiasi. Walidhani awali ni hedhi, lakini dalili za kizunguzungu ziliwatia wasiwasi.
Alilazwa kwa siku tano na kuongezewa damu. Siku ya pili, ripoti ilithibitisha leukemia. Familia ilishauriwa kumpeleka Hospitali ya Aga Khan, na mumewe Hiram Gitau (Tosh) alipanga safari kwenda Amerika kwa matibabu. Betty alikataa ukweli wa ugonjwa huo. Mnamo Oktoba 27, hali yake ilizorota, na alirudishwa RFH. Marafiki waliunda kundi la WhatsApp la watu 30 kumpa moyo.
Kila transfusion ilimpa nguvu kidogo, na alitaka kurudi nyumbani. Shiro alimwita Hiram arejee. Novemba 3, alilazwa Hospitali ya AAR. Baada ya siku mbili, alipata stroke kutokana na kuvuja damu ndani, na akapoteza uwezo wa kuzungumza, ingawa madaktari walizuia hali hiyo. Alishauriwa kuhamishiwa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) katika wodi ya wagonjwa binafsi.
Betty aliomba siri iwe siri; hakutaka picha au michango mtandaoni. “Aliomba tusiposti picha zake wala kuanzisha michango mtandaoni,” Shiro alisema. Kabla ya KNH, aliona watoto wake wawili na alianza kulia bila kuzungumza. Alimba wimbo wake '11th Hour' siku ya mwisho kabla ya kupoteza sauti.
Mwili wake ulikataa damu mpya, ishara ya hatua ya mwisho. Asubuhi ya kifo, wataalamu wa saikolojia waliwaandaa watoto wake. Alifariki Jumatatu, Novemba 10, akiacha watoto wawili na urithi wa muziki wa injili. Maandalizi ya mazishi yanaendelea; wasanii na marafiki wakutana kila siku saa 12 jioni katika Hoteli ya Bluesprings na nyumbani EdenVille Estate, Barabara ya Kiambu.