Serikali ya Kenya imetangaza mpango wa kuoanisha mahitaji ya afya na yale ya kifedha ili kuhakikisha Wakenya wanapata huduma bora za afya chini ya Mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC). Makatibu wakuu kutoka wizara za Afya na Fedha wameahidi kutoa ufadhili wa wakati na kuimarisha miundombinu. Hii inakuja baada ya tangazo la Aprili kwamba milioni 21.3 ya Wakenya wanafaidika tayari.
Alhamisi, Katibu Mkuu anayesimamia huduma za matibabu katika Wizara ya Afya, Dkt Ouma Oluga, na mwenzake wa Wizara ya Fedha, Chris Kiptoo, waliandaa mkutano ili kuhakikisha utekelezaji wa UHC unaoana na mfumo wa kiuchumi unaowainua wananchi wa mapato madogo.
Dkt Oluga alisisitiza kuimarisha hospitali za kiwango cha rufaa, matumizi ya teknolojia katika huduma za kimatibabu, utafiti, uvumbuzi wa kimatibabu na utengenezaji wa chanjo. Aliongeza kuwa huduma bora za afya zitafanikiwa tu ikiwa mgao wa bajeti utatosha na utawasilishwa kwa wakati. “Bajeti finyu na pia ukosefu wa ufadhili unaathiri utoaji huduma kwenye hospitali za rufaa, asasi za utafiti na pia mipango ya afya ya kijamii,” akasema Dkt Oluga.
Bw Kiptoo alisema ufadhili wa kutosha utasaidia kufanikisha UHC na kushusha gharama za matibabu kwa kila Mkenya. Makatibu hao wawili waliahidi mfumo wa kutolewa kwa fedha kwa wakati ili kuepuka pengo linasababisha ukosefu wa huduma.
Hoja kuu ni mageuzi katika ufadhili wa sekta ya afya, mageuzi ya kidijitali, uwekezaji katika sekta ya afya na kurahisishwa kwa upatikanaji wa huduma kwa Wakenya wote. Mnamo Aprili, Waziri wa Afya Aden Duale alitangaza kuwa Wakenya milioni 21.3 wanapata huduma bora chini ya UHC.