Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, ametetea uamuzi wake wa kufungua chumba kipya cha kuhifadhia maiti licha ya kuchelewa kwa miradi mingine ya hospitali. Wakosoaji wanasema anatoa kipaumbele kwa miradi isiyo ya dharura. Wanga anasema huduma hiyo ni muhimu kwa heshima ya mazishi.
Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, alifungua rasmi chumba kipya cha kuhifadhia maiti Alhamisi katika hospitali kuu ya rufaa ya kaunti hiyo. Chumba hicho kina uwezo wa kuhifadhi miili 137, ikiwemo 37 katika sehemu ya watu binafsi. Wanga alisema ujenzi huo ulikuwa ombi la wakazi wakati wa kampeni, kwani mochari ya zamani, iliyojengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, ilikuwa na uwezo wa maiti 20 pekee na mara nyingi ilikuwa imejaa.
“Wakati mwingine mwili wa marehemu ulilazimika kuwekwa juu ya mwingine. Watu wengi walikuwa wanalazimika kupeleka wapendwa wao kwenye mochari za kibinafsi,” alisema Wanga. Aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha mazishi yenye heshima kwa wote. “Wote tutafika mwisho wa safari ya maisha. Ni muhimu tuwape wafu wetu heshima wanazostahili,” alisema.
Hata hivyo, uamuzi huo umekosolewa na baadhi ya wakazi na watumiaji wa mitandao ya kijamii, wakidai kuwa serikali ya kaunti inatoa kipaumbele kwa miradi isiyo ya dharura. Wamehoji kwa nini ujenzi wa jengo la hospitali lenye thamani ya Sh200 milioni, ulioanza Machi 2023, haujakamilika, ilhali makao makuu mapya ya kaunti yalimalizika haraka na kufunguliwa na Rais William Ruto Agosti mwaka huu.
Miongoni mwa wakosoaji ni Odoyo Owidi, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Maendeleo ya Maji Kusini mwa Ziwa Victoria. Kupitia Facebook, Owidi alisema mradi wa mochari ni “anasa” na si kipaumbele.
Wanga alitetea utendakazi wake, akisema serikali yake imeleta mageuzi katika sekta ya afya, ikiwemo kuinua hospitali ya rufaa kutoka ngazi ya 4 hadi 5. “Tulipoingia ofisini mwaka 2022 hospitali ilikuwa ya ngazi ya nne. Kupitia juhudi zetu na msaada wa Wizara ya Afya, tumeweza kuinua huduma na sasa wananchi wanapata matibabu bora,” alisema. Aidha, chumba hicho kitatumika na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu Kenya (KMTC) wanaosoma huduma za mochari.