Wanaume Kisumu waonywa dhidi ya kuwaambukiza HIV wake zao wajawazito

Idara ya Afya ya Kaunti ya Kisumu imeeleza hofu kuhusu wanaume wanaowaambukiza virusi vya HIV wake zao wajawazito kupitia uhusiano wa ngono nje ya ndoa. Hii imetajwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani. Visa vya maambukizi mapya yanazidi kuongezeka katika kaunti hiyo.

Katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Shule ya Msingi ya Kisian, Kaunti Ndogo ya Kisumu Magharibi, Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Fredrick Oluoch, alionya wanaume dhidi ya mwenendo wa kushiriki ngono bila kinga na wapenzi nje ya ndoa. Alisema kuwa wamegundua visa ambapo akina mama hawana virusi vya HIV katika miezi ya kwanza ya uja uzito lakini hupatikana nao wakati wa miezi ya mwisho kabla ya kujifungua. Hii inaashiria uwezekano mkubwa wa maambukizi kutoka kwa waume wao.

"Tunaendelea kushuhudia hali inayotishia ambapo mama hupimwa na kutopatikana na virusi miezi mitatu ya kwanza ya uja uzito na katika miezi tatu ya mwisho kabla ya wao kujifungua, hupatikana na virusi hivyo. Hii ina maana kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba walipata virusi hivyo kutoka kwa waume zao wanaoshiriki mapenzi bila kinga nje ya ndoa," akasema Dkt Oluoch.

Ripoti ya Baraza la Kitaifa la Kudhubiti Magonjwa Sugu (NSCC) inaonyesha Kisumu ni miongoni mwa kaunti zenye viwango vya juu vya maambukizi mapya ya HIV mwaka 2024. Kiwango cha maambukizi ni asilimia 11, na watu 111,367 wanaishi na virusi hivyo. Maambukizi mapya yalifikia 1,341, wakiwemo wanawake 755, wanaume 361 na watoto 225. Visa vya maambukizi kutoka mama kwenda mtoto (MTCT) vilipungua kutoka asilimia 9 mwaka 2019 hadi 5.97 mwaka 2024.

Dkt Oluoch alisema idara yao inalenga kupunguza kiwango hadi chini ya asilimia 5, lakini mienendo ya wanaume inazuia juhudi hizo. "Wanaume hawa wanafaa kuwalinda wake zao waja wazito kwa kukoma kujihusisha katika ngono bila kinga na wapenzi nje ya ndoa. Wanapaswa kuwa watulivu, wawalinde wake zao nyakati za uja uzito," aliongeza.

Tovuti hii inatumia vidakuzi

Tunatumia vidakuzi kwa uchambuzi ili kuboresha tovuti yetu. Soma sera ya faragha yetu kwa maelezo zaidi.
Kataa