Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amefichua jinsi yeye na Naibu Rais Kithure Kindiki walijaribu kumsaidia Rigathi Gachagua kuepuka kuondolewa mamlakani. Aidha, Ruku ametangaza kupinga juhudi za kuunganisha kura za Mlima Kenya nyuma ya Gachagua kuelekea uchaguzi wa 2027. Alisema ushauri wao ulipuuzwa na Gachagua akakataa kufuata maagizo ya kuwa mnyenyekevu.
Katika mahojiano yake kwenye kipindi cha Kimuri cha Inooro TV, Waziri Geoffrey Ruku alielezea kuwa walikaa na Gachagua mara tatu ili kumshawishi awe mnyenyekevu, mtulivu, mwenye heshima na mvumilivu ili kuepuka mashtaka. "Tulikaa naye chini mara tatu. Tulijaribu kumfunza jinsi angeweza kunusurika kama Naibu Rais. Tulimwambia awe mnyenyekevu, mtulivu, mwenye heshima na mvumilivu. Hakusikia," alisema Ruku.
Gachagua, ambaye sasa ni aliyekuwa Naibu Rais, alikiri katika mahojiano yake ya Novemba 22, 2025 na vituo vya redio vya lugha ya Embu kwamba Kindiki alijaribu kusuluhisha mzozo wake na Rais Ruto. "Prof Kindiki alijaribu kuingilia kati mgogoro wangu na Rais. Aliniambia niwe mvumilivu na mtiifu, niwe mnyenyekevu na niunge mkono rais. Nikakataa. Nilimwambia haiwezekani niwe sehemu ya utekaji watu na mauaji nje ya sheria," alisema Gachagua.
Ruku aliongeza kuwa Gachagua aliruhusu kiburi na ubabe vitawale, na hivyo akalazimika kutimuliwa baada ya miaka miwili afisini. "Badala ya kusikiliza hekima, Bw Gachagua aliruhusu kiburi, ubabe na dharau vitawale katika miaka yake miwili afisini, na hatimaye akalazimika kutimuliwa," alisema.
Kwa sasa, Gachagua anadai hajutii kuondolewa kwake na ana azma za kuunganisha Mlima Kenya, kukuza viongozi vijana na kumwondoa Ruto mamlakani 2027. Hata hivyo, Ruku ametangaza kupinga hilo vikali. "Mradi Gachagua yuko kwenye picha, Mlima Kenya lazima ugawanyike. Ni heri tugawanyike ikiwa hilo litahakikisha tunabaki serikalini," alisema. Alisisitiza kuwa kaunti za Meru, Embu, Tharaka Nithi na sehemu za Kirinyaga zinapaswa kuungana kumpa Ruto angalau kura milioni mbili 2027.
Ruku aliongeza kuwa Rais Ruto ataanza ziara kubwa eneo la Mlima Kenya kuanzia Mwaka Mpya ili kuzindua miradi ya maendeleo na kuimarisha uungwaji mkono. "Hii ni serikali yetu. Mlima Kenya una uwakilishi mkubwa zaidi serikalini mawaziri, makatibu wakuu na nyadhifa nyingine. Sisi ndio tumepokea mgao mkubwa wa maendeleo. Haiwezekani mtu aseme Rais Ruto ni adui wetu," alisema. Alionya wapiga kura dhidi ya kufuata Gachagua, akirejelea matokeo ya uchaguzi mdogo wa Mbeere North.