Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli amelalamikia Wakenya wanaotafuta ajira ng'ambo kwa njia za haramu na kuishia kulaumu serikali. Pia amewahimiza wafuate taratibu rasmi na kuwaondoa maajenti wakora. Aidha, amewalaumu wanaharakati kwa kupeleka uanaharakati Uganda na Tanzania.
Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) na Rais wa Muungano wa Wafanyakazi Afrika (OATUU), amelalamikia idadi ya Wakenya wanaotoka nchini kutafuta ajira ng'ambo na kuishia kukwama huko. Kulingana na taarifa yake, baadhi ya hawa hutumia njia za mkato kisha wakikamatwa na kuanza kulilia serikali, hasa Wizara ya Mambo ya Nje.
Atwoli aliwataka Wakenya wahakikishe kuwa wanafahamisha ubalozi wa Kenya katika nchi husika ili kuepuka matatizo. "Kenya inaendelea kujiweka kama taifa ambalo linatoa raia wake kufanya kazi katika mataifa ya nje. Hata hivyo, ni vyema iwapo kutakuwa na rekodi yao na pia watambuliwa kupitia asasi zilizopo za serikali. Hii itahakikisha wanasaidiwa iwapo kuna tatizo ambalo litatokea badala ya kuachwa wakihangaika na maajenti wenye tamaa ya hela," alisema Atwoli.
Pia, Atwoli amewalaumu wanaharakati Wakenya kwa kupeleka uanaharakati Uganda na Tanzania, na hivyo kukiuka kanuni za kimataifa. "Nashangaa kuwa baadhi ya Wakenya sasa wanalaumu serikali hasa Wizara ya Masuala ya Nje wakikamatwa mataifa wanakopeleka uanaharakati wao. Hii ni licha ya kwamba wakienda mataifa hayo huwa hawafuati utaratibu unaohitajika kwa sababu wanajua wana hila," aliongeza.
Kwa zaidi ya miezi sita iliyopita, COTU imepokea malalamishi kutoka kwa Wakenya wanaofanya kazi nje kuhusu wanaharakati hawa wanaovuruga udhabiti wa nchi hizo. Atwoli alionya kuwa hii inawahatarisha raia hao na kuwapaka doa serikali. "Wanaoenda nje wasiwachochee Wakenya au kutaka wahurumiwe kwa sababu hakuna aliyefahamu sababu zao za kuondoka Kenya na kupeleka uanaharakati wao katika nchi hizo," alisema.
Atwoli alisisitiza kuwa Kenya haivumilii uingiliaji kati kutoka nje, hivyo wanaharakati wa ndani wasifanye hivyo mataifa mengine. "Wafanyakazi wote wanastahili kufuata sheria za Kenya kila mahali walipo ndipo hata maslahi yao yatalindwa. Kama Cotu tutaendelea kulinda hadhi ya mfanyakazi Mkenya kila mahali yupo," alihitimisha.