Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na makamu wa rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Mwaura Kabata wamewasilisha kesi mahakamani ili kuwazuia mawaziri kushiriki kampeni za kisiasa. Wanadai kuwa hii inakiuka wajibu wa afisi yao wa kutokuwa na upendeleo. Wanataka mahakama ibaini kuwa sehemu ya 25 ya Sheria ya Mgongano wa Kimamlaka ya 2025 ni kinyume cha Katiba.
Babu Owino na Mwaura Kabata wamefika Mahakama Kuu wakidai mawaziri wa serikali ya kitaifa na wale wa kaunti wazuiwe kushiriki shughuli za kisiasa. Wanasisitiza kuwa kushiriki kampeni kunakiuka Kipengele cha 75 cha Katiba, kinachowahitaji maafisa wakuu wa serikali kuonyesha mienendo isiyo na mgongano kati ya maslahi ya kibinafsi na majukumu ya umma.
Kulingana na kesi hiyo, Sehemu ya 25 ya Sheria ya Mgongano wa Kimamlaka Nambari 11 ya 2025 inawaruhusu mawaziri kupinga au kuunga mkono masilahi ya vyama vya kisiasa, au kushiriki shughuli zinazoathiri upendeleo wa afisi zao. Walalamishi hawa wanasema hii inabagua maafisa wengine wa serikali ambao wanazuiwa kushiriki siasa chini ya Sheria ya Utawala Bora na Maadili ya 2012, Sehemu ya 23(2), inayowazuia kuingilia hitaji lao la kutokuwa na upendeleo.
Wanadai zaidi ya mawaziri 20 wamenaswa na vyombo vya habari wakishiriki kampeni, wakitafuta uungwaji mkono kwa wagombeaji katika chaguzi ndogo za Novemba 27, 2025. “Kwamba kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, Mahakama hii inaombwa kutoa agizo la kuzuia kutumika kwa Sehemu ya 25 ya Sheria ya Mgongano wa Kimasilahi Nambari 11 ya 2025,” Kabata alisema.
Walalamishi wanaeleza kuwa mamlaka ya maafisa wakuu ni kwa manufaa ya umma na inahitaji kuendeleza uaminifu machoni pa umma. Wanataja tukio la Aprili 2, 2025, wakati wa mkutano wa Rais William Ruto huko Kieni, Nyeri, ambapo Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alidaiwa kuhusisha Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na siasa. Wanasisitiza kuwa maafisa wanawajibika kuwahudumia wananchi, sio kuwatawala.