Washukiwa wanne wakamatwa kisumu kwa kuiba bastola ya mlinzi wa gavana barasa

Polisi wa Kisumu wamewakamata washukiwa wanne na kukomboa bastola moja iliyonyang'anywa mlinzi wa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa wakati wa mazishi ya Raila Odinga. Washukiwa walikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa umma, na wanatarajiwa kushtakiwa mahakamani. Bastola hiyo ilipatikana ikiwa na risasi 14.

Kulingana na taarifa ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliyotolewa jana, maafisa wa polisi walivamia nyumba moja katika kitongoji cha Manyatta “B” eneo la Mbeme, Kaunti Ndogo ya Kisumu Mashariki, na kuwakamata washukiwa wanne. Walitambuliwa kama Timothy Odhiambo, David Beckham Odhiambo, Tony Blair Omondi na Harun Ibrahim.

Baada ya kuhojiwa, washukiwa waliwaongoza maafisa hadi maficho mengine ambapo walipata bastola aina ya Jericho ikiwa na risasi 14. “Uchunguzi umebaini kuwa bastola iliyopatikana ni ile iliyonyang’anywa afisa mmoja wakati wa mazishi ya Mheshimiwa Raila Amolo Odinga mnamo Oktoba 19, 2025 Bondo, kaunti ya Siaya. Washukiwa hao wanazuiliwa kabla ya kuwasilishwa kortini kujibu mashtaka,” DCI ilisema kwenye taarifa yake kwenye akaunti ya X.

Bastola hiyo ilinyang'anywa afisa wa GSU, ambaye alikuwa mmoja wa walinzi wa Gavana Barasa, wakati wa mazishi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) huko Bondo. Afisa huyo alipokuwa akiondoka na wenzake na bosi wao, alitoweka ndani ya umati mkubwa wa watu waliohudhuria ibada. Duru zilisema wahuni waliwapora mali ya watu kadhaa wakati na baada ya ibada hiyo iliyovutia waombolezaji kutoka nchini na nje.

Tovuti hii hutumia kuki

Tunatumia kuki kwa uchambuzi ili kuboresha tovuti yetu. Soma sera yetu ya faragha sera ya faragha kwa maelezo zaidi.
Kataa