Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesajili wapiga kura wapya 90,020 kufikia Oktoba 31, 2025. Mwenyekiti Erastus Ethekon alitangaza hii Novemba 2, 2025, akisema inaonyesha maendeleo katika zoezi lililoanza Septemba 29. Nairobi inaongoza na 16,512 wapya, ikifuatwa na Kiambu.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa imesajili jumla ya wapiga kura wapya 90,020 kufikia Oktoba 31, 2025. Tangazo hili lilitolewa Novemba 2, 2025, na mwenyekiti wa tume, Erastus Ethekon, katika taarifa kwa vyombo vya habari. Ethekon alisema idadi hii inaonyesha hatua nzuri katika zoezi la usajili lililoanza kote nchini Septemba 29, isipokuwa katika maeneo 24 ambapo chaguzi ndogo zitaendeshwa Novemba 27.
Kulingana na Ethekon, kaunti ya Nairobi inaongoza kwa kuwasajili 16,512 wapiga kura wapya, ikifuatwa na Kiambu yenye 9,917 na Machakos 4,026. Kaunti zingine zilizoandikisha zaidi ya 3,000 ni Mombasa (3,967), Kitui (3,552), Murang’a (3,330), Nakuru (3,265) na Meru (3,128).
Kwa upande mwingine, kaunti za Tana River, Isiolo, Samburu, Nyamira, Marsabit na Elgeyo Marakwet zimesajili chini ya 400 wapiga kura wapya tangu zoezi lilipoanza, na Tana River ikiwa na 130 pekee. Ethekon alielezea kufurahishwa kwake na idadi hii, akisema inaashiria kujitolea kwa IEBC kutimiza wajibu wake kulingana na Katiba.
“Hatu hii inaakisi kujitolea kwa IEBC kutimiza wajibu wake kulingana na kipengele cha 88 (4) cha Katiba wa kufanikisha usajili wa wapiga kura katika maeneo bunge yote 290,” alisema Ethekon. “Aidha, raia wanajitokeza kubadilisha vituo vyao vya kupigia kura na maelezo yao kwenye sajili ya wapiga kura ishara kwamba wanatambua umuhimu wa shughuli hii itakayowawezesha kuwachagua viongozi wanaowataka.”
IEBC ilitoa wito kwa wadau kuwahimiza raia kujisajili, kuthibitisha maelezo yao na kuhamia vituo vya kupigia kura wanavyotaka.