Wakazi wa kijiji cha Kokuro, Kaunti ya Turkana, waliripoti wizi wa punda zaidi ya 100 kupitia mfumo wa kidijitali na wakapata msaada wa haraka kutoka maafisa wa usalama.
Mwezi uliopita, wavamizi wenye silaha waliiba punda zaidi ya 100 katika kijiji cha Kokuro kilichopo mpakani mwa Kenya na Ethiopia. Badala ya kuanza msako wa muda mrefu, wakazi walitumia Kituo cha Kidijitali cha Habari za Punda kuripoti tukio hilo.
Taarifa zilifika haraka kwa maafisa na punda wakapatikana. Programu ya Punda Wangu inatumia Akili Unde kusajili punda kwa picha na alama zao maalumu ili kurahisisha utambuzi.
Mfumo huo pia unaruhusu wafugaji kuripoti magonjwa na ukatili bila malipo. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Kuhusu Ufugaji wa Kuhamahama, Mariko Akileng, alisema mfumo unalenga kuunganisha wafugaji na polisi kwa hatua za haraka.