Nairobi yaongoza kitaifa kwa maambukizi mapya ya HIV kwa mara ya kwanza

Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, Kaunti ya Nairobi imeipiku Homa Bay na kuongoza kitaifa katika idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya HIV. Ripoti ya Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Kuambikizana (NSDCC) inaonyesha ongezeko la maambukizi kitaifa na idadi ya vifo. Hii imetokea siku moja kabla ya Siku ya Ukimwi Duniani.

Kulingana na data ya NSDCC, Nairobi iliandikisha maambukizi mapya 3,045 ya HIV mwaka 2024, ikipiku Homa Bay. Migori ilikuwa ya pili na 1,572 maambukizi, ikifuatwa na Kisumu yenye 1,341. Kwa miaka mingi, kaunti za Homa Bay, Migori, Kisumu na Siaya zimekuwa zikiongoza.

Maambukizi mapya kitaifa yaliongezeka kwa asilimia 19, kutoka 16,752 mnamo 2023 hadi 19,991 mwaka 2024. Kaunti 10, ikiwa ni pamoja na Nairobi, Migori, Kisumu, Homa Bay, Busia, Siaya, Kakamega, Nakuru, Mombasa na Bungoma, zilichangia asilimia 60 ya maambukizi hayo. Kiwango cha maambukizi kitaifa kilikuwa 3.0%, na wanawake 4.0% dhidi ya wanaume 2.0%.

Ripoti ya "Kenya HIV Estimates" iliyotolewa na NSDCC inaonyesha kuwa vifo kutokana na Ukimwi viliongezeka hadi 21,007 mwaka 2024, kutoka 18,473 mnamo 2023. "Jumla ya vifo 21,000 vinavyotokana na Ukimwi vilivyoandikishwa mnamo 2024, inatukumbusha kuhusu haja ya juhudi kuongezwa kuwahamasisha watu kupimwa mapema, kuzingatia taratibu za matibabu na utunzaji watu wanaoishi na ukimwi," akasema Katibu wa Afya ya Matibabu Ouma Oluga.

Hata hivyo, idadi ya Wakenya wanaoishi na HIV ilipungua hadi 1,326,336, ikiwa na watoto 62,798. Maambukizi mapya yanabaki juu miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 34. Aidha, maambukizi mapya yalipungua kwa asilimia 75 katika kaunti kama Elgeyo-Marakwet, Wajir, Mandera, Kisii, Machakos, Kericho, Uasin Gishu, Nakuru, Bomet, Baringo, Trans-Nzoia na Laikipia, ingawa Nakuru pia iko katika orodha ya kaunti 10 zinazoongoza maambukizi.

Tovuti hii inatumia vidakuzi

Tunatumia vidakuzi kwa uchambuzi ili kuboresha tovuti yetu. Soma sera ya faragha yetu kwa maelezo zaidi.
Kataa