Rais William Ruto amezindua mpango wa NextGen Youth Empowerment Programme wenye thamani ya Sh2 bilioni ili kuwapa vijana mafunzo na ajira.
Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na sekta ya kibinafsi. Unalenga kuwapa vijana ujuzi wa kazini na uzoefu unaohitajika katika soko la ajira.
Rais Ruto alisema serikali inawekeza katika mipango inayounganisha elimu na ajira. Alisema mafunzo kazini si kazi za muda tu bali ni daraja kati ya kujifunza na kujipatia kipato.
Serikali imerekodi mafanikio kama kuajiri vijana 100,000 kama walimu na kuwafunza zaidi ya milioni 1.9 ujuzi wa kidijitali. Hii imechangia kuundwa kwa nafasi za kazi 350,000 katika sekta hiyo.