Makamu wa Rais wa Amerika JD Vance anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Kenya kati ya Novemba 25 na 30. Ziara hii inafanyika wakati nyeti kwa uhusiano wa kibiashara na kiusalama kati ya Kenya na Marekani. Serikali ya Rais William Ruto inatumaini kufufua uhusiano wa karibu ulioshuhudiwa wakati wa utawala wa Joe Biden.
Ziara ya Makamu wa Rais JD Vance inaweka Nairobi tena katika jukwaa la kidiplomasia la kimataifa, takriban mwaka mmoja na nusu tangu Rais William Ruto afanye ziara ya kihistoria nchini Amerika Mei 2024. Wakati huo, Kenya ilipandishwa hadhi na kutambuliwa kama “Mshirika Mkuu wa Amerika asiye mwanachama wa NATO” (MNNA), taifa la kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata hadhi hiyo, ikiiweka katika nafasi ya kipekee kama mshirika wa karibu wa Amerika katika masuala ya kijeshi na kiusalama.
Ingawa Ikulu ya Nairobi imekuwa kimya kuhusu maelezo, mazungumzo ya ngazi ya juu yameendelea kati ya maafisa wa nchi hizo mbili. Waziri wa Masuala ya Kigeni na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, alisema: “Kwa mwaka uliopita, ahadi nyingi zilizotolewa sasa zimeanza kutekelezwa kwa vitendo na maendeleo ni ya kuridhisha.” Aidha, Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei, aliongeza kuwa ziara inaonyesha uthabiti wa uhusiano na mwendelezo wa mazungumzo yaliyoanza baada ya ziara ya Ruto, heshima ambayo haikuwa imetolewa kwa kiongozi yeyote wa Afrika kwa zaidi ya miaka 20.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa chama cha Republican wamependekeza hadhi ya MNNA ipitiwe upya, wakitaja uhusiano wa Kenya na China, Urusi na Iran. Mwezi Agosti, Seneta Jim Risch aliwasilisha mswada bungeni kutaka tathmini upya, akitaja biashara na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu. Mudavadi alidhibitisha kuwa ushirikiano umeendelea vizuri, na mazungumzo mapya yanajumuisha teknolojia ya utengenezaji wa vipuri vya kielektroniki na madini adimu.
Biashara ni ajenda kuu, hasa kuhusu Mkataba wa AGOA unaoisha Septemba 2026. Utawala wa Donald Trump uliongeza mpango huo kwa mwaka mmoja ili Kenya iweze kujadiliana makubaliano mapya. Mudavadi alisema: “Iwapo Amerika haitadumisha AGOA kwa nchi zote, basi kila nchi italazimika kujadiliana masharti yake binafsi.”
Ziara pia inahusu Operesheni ya Amani nchini Haiti, ambapo Kenya imetuma maafisa wa polisi 800, lakini mpango unakabiliwa na ukosefu wa ufadhili baada ya Marekani kuashiria kuweza kuasitisha mchango wake wa dola milioni 200. Hii inafanyika wakati Washington ina wasiwasi kuhusu ushawishi unaoongezeka wa China barani Afrika, hasa baada ya ziara ya Ruto nchini Beijing Aprili, ambapo walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia. Wachambuzi wanasema ziara ya Vance italenga kuweka Kenya kama nguzo ya kimkakati ya Amerika katika biashara, ulinzi na usalama wa kikanda.