Ukosefu wa ajira umesababisha vijana wengi kuingizwa katika biashara haramu za ngono, huku polisi wakifanya uvamizi mwingi katika kaunti mbalimbali.
Katika mwezi mmoja uliopita, maafisa wa polisi walivamia nyumba katika kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado na Nakuru na kuwaokoa zaidi ya wanawake 50 waliolazimishwa kutengeneza filamu za ngono.
Wiki nne zilizopita, polisi walivamia eneo la Ngoigwa, Thika, na kukamata vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 30 pamoja na vifaa vya kurekodi. Miezi michache kabla, Idara ya Upelelezi wa Jinai ilivunja mtandao mwingine Nakuru na kukamata mfanyabiashara aliyewavutia wasichana wa shule.
Mnamo Julai 21, DCI iliwaokoa wanawake watano katika Mihang’o, Embakasi Mashariki. Siku tatu baadaye, wanawake wengine 48 waliokolewa Ongata Rongai na Kiserian. Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin alisema waathiriwa walidanganywa kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono.