Mamlaka ya Huduma za Hali ya Anga nchini Kenya imewatahadharisha wakulima kuhusu hali ya ukame na jua katika sehemu nyingi za nchi mwezi wa Julai.
Kulingana na taarifa ya Julai Farming Outlook iliyotolewa Julai 5, unyevu wa udongo utapungua kwa kasi katika maeneo mengi kutokana na hali ya ukame inayotarajiwa.
Kenya Met ilisema kuwa hali kavu itasaidia wakulima kuvuna, kukausha na kuhifadhi mazao yaliyokomaa kama mahindi katika kaunti za Magharibi kama Kakamega na Bungoma pamoja na Machakos na Embu.
Hata hivyo, kaunti za Pwani kama Kilifi na Kwale zinatarajiwa kupata mvua ya kawaida au zaidi, huku Nyanda za Juu za Kati na Nairobi zikipata manyunyu mepesi mara kwa mara.
Wakulima wameshauriwa kutumia mbinu za kuhifadhi unyevu kama kufunika udongo na kumwagilia mazao yanayobaki shambani. Joto litakuwa juu zaidi ya kawaida isipokuwa katika maeneo ya Nyanda za Juu za Kati.