Wakazi wa eneo bunge la Mbeere North, Kaunti ya Embu, wamelalamikia kuondolewa kwa transfoma za umeme miezi minane baada ya kuunganishwa kupitia mpango wa Last Mile Connectivity.
Wakazi wanasema walipata umeme kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi mdogo wa Novemba 27, 2025. Faith Kithaka wa kijiji cha Muramba alisema maafisa wa Kampuni ya Kusambaza Stima Kenya waliondoa transfoma wiki mbili zilizopita.
Wakazi walidai kuwa hatua hiyo imewarudisha katika maisha ya kutumia mishumaa na taa za mafuta. Julius Njeru wa kijiji cha Rwanjeru alisema biashara na masomo ya watoto yameathirika.
Mbunge Leo Wamuthende alikanusha madai hayo na kusema KPLC inafanya matengenezo ya kawaida. Meneja wa KPLC Kaunti ya Embu Vincent Okello alisema transfoma tatu ziliharibiwa na zilipelekwa Nairobi kutengenezwa.