Wataalamu wa mahusiano wanasema kuwa ingawa mawasiliano ya wazi ni muhimu, si kila siri inapaswa kushirikiwa mara moja katika uhusiano mpya. Kuficha mambo fulani kunaweza kulinda imani na uthabiti. Hii inaweza kuzuia wivu, hasira na kuvunjika kwa uhusiano.
Katika mahusiano ya mapenzi, ushirikiano na mawasiliano ya wazi ni muhimu, lakini si kila kitu unachofahamu kumhusu mchumba wako au maisha yako unapaswa kumwambia mara moja. Watu wengi wanadhani kuwa ukweli wote unapaswa kusemwa wanapoanza uhusiano wa kimapenzi, lakini wataalamu wanasema kwamba mambo fulani yanapofichwa au kukosa kusemwa, yanaweza kulinda imani, thamani na uthabiti wa uhusiano.
Kulingana na mtaalamu wa mahusiano Dkt John Gottman, kumkosoa mpenzi mara kwa mara kunadhoofisha misingi ya imani na upendo katika uhusiano wenu. “Pili, kuanika faragha kuhusu wapenzi wa zamani ni hatari kwa sababu inaweza kuzua wivu au hisia za kutokuwa na usalama. Uhusiano unahitaji hisia za kuaminiana, na kufungua historia ya mapenzi ya zamani bila sababu inaweza kuharibu hiyo misingi,” asema Gottman. Mtaalamu huyu anasema kwamba kusalia na historia ya hisia za zamani kunaweza kumfanya mpenzi wako ajihisi hatarini au kushindwa kukuamini. “Zika mahusiano ya zamani katika kaburi la sahau iwapo unataka kulinda ndoa au uhusiano wako mpya,” asema Gottman.
Aidha, siri zinazoweza kuhatarisha uhusiano kama madeni yaliyofichwa, makosa ya kifedha, au tabia zinazoweza kuvunja imani zinapaswa kushughulikiwa kwa makini. “Kuanika mambo haya bila mpangilio au kuyaficha kabisa, kunaweza kusababisha hasira, kutoelewana, kupungua kwa imani au hata kuvunjika kwa uhusiano,” asema Gottman.
Umbea kuhusu marafiki au familia ni sumu nyingine hatari kwa uhusiano. Kulingana na Dkt Terri Orbuch, mtaalamu wa mahusiano, kufichua mambo ya faragha kwa watu wengine kunapunguza heshima ya mpenzi kwa uhusiano wenu. Pia, hofu au udhaifu wa kibinafsi inapaswa kushughulikiwa kwa uangalifu. “Mpenzi wako huenda asielewe mara moja hisia zako nzito, na kumwambia kila kitu kwa wakati mmoja kunaweza kuunda mchanganyiko wa kihisia. Ufahamu wa polepole wa udhaifu wa mwenzako huongeza imani na upendo wa kweli,” asema Terri.
Mipango mikubwa au maamuzi ya maisha kama kuhama, kuacha kazi au mabadiliko makubwa bila kujadiliana na mchumba wako inaweza kuleta mvutano. Malalamishi yanayoumiza kama kusema “mpenzi wa rafiki yangu ni bora kuliko wewe” yanaweza kuunda hisia za kudunisha na za chuki. “Ni muhimu kuelewa mambo ambayo yanaweza kuhatarisha uhusiano au imani ya mchumba wako na kufahamu namna na wakati ufaao kuyasema. Kuyatoa uhusiano ukiwa imara na kila mmoja wenu akiwa tayari kwa mazungumzo ya wazi ni bora ili kulinda upendo, imani na heshima miongoni mwa wanandoa,” asema Terri.