Mbunge wa Embakasi Mashariki David Gikaria alipewa muda wa saa saba unusu kufika mbele ya Kamati ya Maadili na Nidhamu ya IEBC baada ya madai ya kutoa hongo wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.
Kamati hiyo inayoongozwa na Dkt Alutalala Mukhwana ilisitisha shughuli zake baada ya Gikaria kutuma msaidizi wake Joseph Kariuki Nelima badala yake. Dkt Mukhwana alisema hawakuridhishwa na sababu zilizotolewa kuhusu kutokuwepo kwa mbunge huyo.
Gikaria alidai kuwa alikuwa mgonjwa na alikuwa na miadi na daktari wake. Pia alisema hakupokea malalamishi yoyote rasmi na alifahamu suala hilo kupitia mitandao ya kijamii.
Inadaiwa mbunge huyo alishiriki katika utoaji wa hongo kwa wapigakura alipokuwa akimfanyia kampeni mgombeaji wa UDA Samuel Muchina Nyaga katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.