Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) limetangaza kuwa wanafunzi wasio na vyeti vya KCPE lazima wathibitishe sifa zao na kufanya mtihani maalum ili waweze kujiandikisha kwa KCSE mwaka 2027.
KNEC ilisema wanafunzi wote wanaonuia kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2027 bila cheti cha KCPE watawasilisha uthibitisho wa elimu ya msingi kwanza.
Mtihani wa kufuzu utafanyika Septemba 2026, na usajili wake utafungwa Julai 30, 2026. Ada ya uthibitishaji ni Sh3,480 na ada ya mtihani ni Sh3,000.
Mkurugenzi Mkuu wa KNEC Dkt David Njengere alisema KCSE ya 2027 itakuwa ya mwisho chini ya mfumo wa 8-4-4 kabla ya mpito kamili kwenda mfumo wa CBE mwaka 2028.
Wanafunzi watahitaji kuwasilisha barua ya maombi, ripoti za shule na nyaraka zingine zinazohitajika.