Wanafunzi wanaoingia gredi 10 mwezi ujao nchini Kenya watahitaji walimu 58,590 zaidi chini ya mtaala wa CBC. Masomo ya STEM yameathiriwa zaidi, na upungufu wa walimu 35,111. Mkurugenzi wa TSC ametoa maelezo kuhusu hitaji hili.
Kutokana na mabadiliko ya mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC), nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na gredi 10 mwezi ujao. Idadi ya wanafunzi 569,000 wamechagua masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM), na hivyo kuhitaji walimu 35,111. Masomo ya sayansi ya kijamii yanahitaji walimu 14,630, wakati yale ya sanaa na michezo yanahitaji 8,778.
Mkurugenzi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC) anayesimamia ubora wa elimu, Dkt Reuben Nthamburi, alisema kuwa upungufu huu umetokana na mfumo mpya wa elimu. “STEM itakuwa na asilimia 60 ya wanafunzi ambao ni 677,144 kwenye madarasa 15,046. Tulifanya hesabu kwa kutumia darasa ambalo lina wanafunzi 45 ambapo tunawahitaji walimu 35,111. Kwa sayansi ya kijamii tunawahitaji walimu 14,630 kisha sanaa na michezo inahitaji 8,778 ambapo idadi ya jumla ni 58,519,” akasema Dkt Nthamburi.
TSC imetoa wito kwa vyuo vikuu na vyuo vya ualimu ili kuhakikisha mafunzo yao yanapatana na mahitaji ya soko, hasa katika masomo ya sanaa na michezo. Dkt Nthamburi alisisitiza umuhimu wa kuwapatia walimu kutosha ili kutoa elimu bora, hasa kwa idadi kubwa ya wanafunzi waliovutiwa na STEM kati ya milioni 1.1 ya wanafunzi katika gredi ya nne. Hii itasaidia kutoa elimu yenye ubora chini ya CBC.