Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen amekosolewa vikali na viongozi wa upinzani kutokana na matamshi yake dhidi ya Rigathi Gachagua.
Viongozi wa Muungano wa Upinzani wakiwemo Kalonzo Musyoka, Justin Muturi na Eugene Wamalwa walitoa shutuma hizo jana wakati wa ibada katika Kanisa la AIC Namanga, Kajiado.
Muturi alimtaja Murkomen kama aliyetekwa na mamlaka na kusema ofisi ilimfanya awe mlevi wa madaraka. Musyoka alisisitiza kuwa matamshi ya Murkomen yanawakilisha msimamo wa Ikulu na kwamba vitisho kwa wananchi na vyombo vya habari havikubaliki.
Murkomen alitoa matamshi yake Jumamosi huko Moiben na jana huko Bungoma, akidai Gachagua hana uwezo wa kutikisa serikali na kwamba nchi iko thabiti chini ya Rais William Ruto.
Upinzani pia ulitangaza mipango ya kuadhimisha Saba Saba tarehe 7 Julai ili kutetea haki za binadamu.