Mbunge wa Kuresoi Kaskazini Alfred Mutai bado anasakwa na polisi kuhusiana na ghasia zilizotokea wikendi kati ya wafuasi wake na wale wa Gavana wa Nakuru Susan Kihika.
Ghasia hizo ziliwaacha watu watano wakiwa na majeraha ya risasi katika eneobunge la Kuresoi Kaskazini. Polisi walikamata zaidi ya vijana 56 wanaoshukiwa kushiriki katika ghasia hizo Shule ya Sekondari ya Umoja, Tulwet.
Bw Mutai amekanusha kuhusika na ghasia hizo na kusema analengwa kisiasa. Yeye ni mbunge wa muhula wa kwanza baada ya kumshinda aliyekuwa Naibu Spika Moses Cheboi kupitia UDA mnamo 2022.
Bi Kihika na wanasiasa wengine walikuwa wakifanya mkutano wa kuchangisha fedha katika wadi ya Nyota. Vijana 44 waliachiliwa huru kutokana na ukosefu wa ushahidi huku 12 wakisalia rumande na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu.