Zaidi ya wiki moja baada ya vurugu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou kuwaua watu wawili na kujeruhi wengine kadhaa, hakuna mshukiwa aliyetiwa mbaroni licha ya maagizo ya Rais William Ruto.
Timu maalumu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai iliyoundwa kuchunguza kisa hicho haikuondoka Nairobi kufikia Jumatano jioni. Maafisa walisema walikuwa bado wakisubiri maagizo kutoka kwa wakubwa wao.
Rais Ruto alizungumza Jumatatu na kuagiza idara za usalama kutekeleza sheria bila upendeleo dhidi ya magenge ya wahuni. Naibu Rais Kithure Kindiki aliunga mkono kauli hiyo siku iliyofuata na kuonya wanasiasa dhidi ya kufadhili magenge hayo.
Kuchelewa huko kunajiri licha ya picha, video na nambari za usajili za magari yanayodaiwa kutumiwa na wahuni kusambazwa mitandaoni.