Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewataka wakazi wa eneo la Magharibi kujisajili kama wapigakura ili wamuunge mkono Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Wetang’ula alitoa wito huo wakati wa hafla ya kuchangisha fedha katika eneo la Kimang’eti, Kaunti Ndogo ya Malava. Alisema eneo la Magharibi linapaswa kumpa Rais Ruto muhula wa pili kutokana na miradi ya maendeleo iliyoletwa na serikali yake.
Alitaja ujenzi wa hospitali mbili za kiwango cha sita katika kaunti za Kakamega na Bungoma kama miongoni mwa miradi hiyo. Hospitali hizo zitawawezesha wakazi kupata matibabu maalumu karibu na makazi yao badala ya kusafiri hadi Eldoret au Nairobi.
Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alihimiza wakazi kutumia zoezi la sasa la uandikishaji wa wapigakura. Alitaja lengo la kaunti hiyo kuwa na wapigakura milioni 1.5 pamoja na kaunti nyingine za Magharibi ili kufikia takriban milioni nne kwa jumla.