Viongozi wa ODM katika Kaunti ya Nairobi wamewataka wafuasi wao wasishiriki maandamano ya Saba Saba yaliyopangwa kufanyika Jumatatu. Wakisema Jumapili, viongozi hao walisema njia ya kutatua changamoto ni mazungumzo badala ya maandamano.
Mbunge wa Makadara George Aladwa, ambaye ni Mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi, alisema hakuna mwanachama wa chama atakayehusika katika ghasia. Alisema wote wako katika Serikali Jumuishi na hawataingia barabarani kwa maandamano hayo.
Aladwa aliwataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Katibu Dkt Raymond Omollo kulinda amani ya nchi. Alitetea Omollo akisema anapaswa kuendelea na kazi yake hadi 2027 bila kuingiliwa.
Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na waliunga mkono uongozi wa Dkt Oburu Oginga katika ODM.