Serikali imeshtakiwa Mahakama Kuu Nairobi kwa madai ya kushindwa kulipa fidia ya bima ya zaidi ya Sh20 bilioni kwa familia za watumishi wa umma waliofariki au kujeruhiwa kazini.
Kesi hiyo imewasilishwa na John Gitonga ambaye anadai serikali imekiuka sheria kwa kushindwa kutoa bima ya lazima na kulipa fidia kwa vifo na majeraha ya kazini. Walioshtakiwa ni pamoja na Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Afya ya Jamii, Mamlaka ya Kudhibiti Bima na Hazina ya Pensheni wa Watumishi wa Umma.
Gitonga anakadiria kuwa serikali inadaiwa Sh8.4 bilioni kwa watumishi wa umma, Sh3 bilioni kwa polisi na magereza na Sh10 bilioni kwa walimu. Anasema madai hayo yanatokana na bima za ajali kazini na fidia chini ya Sheria ya Fidia kwa Majeraha Kazini.
Katika kiapo chake Gitonga anasema aliamua kwenda mahakamani baada ya dadake aliyekuwa mfanyakazi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu kufariki kazini na watoto wake kukosa mafao ya bima. Anataka mahakama itangaze mpango huo kuwa kinyume cha katiba na iamuru malipo ya madai yote.